Amani akiwa katika moja ya kazi zake |
Ni muda wapita sasa amekuwa akingojea ndoto zake zitimie...Mungu mwema jamani amekwenda kumtimizia kijana huyo ndoto zake kwa Tamasha kubwa la maonyesho ya makabila mbalimbali litakalowika kuanzia Septemba 6-8 mwaka huu, huko Haydom.
Tamasha hilo limeweza kushirikisha makabila mbalimbali, na kutakuwa na mashindano ya ngoma za asili kwani makundi zaidi ya 18 ya Ngoma za Wanyiramba, Wanyisanzu, Wairaqw, Wadatooga na Wahadzabe watachuana vilivyo kwenye tamasha hilo.
Mwandishi wa blog ya Reallife4Christian aliweza kulonga na mwandaaji wa Tamasha hilo mwenye maono ya kufika mbali akiwa katika umri mdogo AMANI PAUL NANAGI ...ni kijana MWIRAQW, kwa njia ya simu na kusema kwamba mbali na mashindano hayo ya ngoma kutakuwa na mashindano ya riadha kwa wazee zaidi ya miaka 50.
akiwa kikazi zaidi |
Alisema mbali na hayo pia kutakuwa na zoezi la kuchangia damu, huku Makampuni mbalimbali yatashiriki kwa kuonyesha bidhaa zao mbalimbali.
"Nimekuwa nikilisubiria kwa muda zaidi ya miaka 8 huku nikiliota tamasha hilo, kwamba ipi siku litafanyika na ndivyo ilivyo tokea kwangu sasa", alisema Amani.
WAIRAQW NI WATU GANI?
Wairaqw ni moja ya makabila matatu tu Tanzania ambayo ni jamii ya Wakushi au Wahamitiki wenye asili yao kwenye nchi za Ethiopia tofauti na wengi wanavyoamini kuwa asili yao ni Mesopotamia yaani Iraq ya sasa(mengine ni Wambugu waliopo Tanga na Wagorowa au wafyomi waliopo Babati).
Utafiti wa kiathropolojia na hata vinasaba (DNA) uliofanyika unathibitisha kuna uhusiano mkubwa kati ya Wairaqw na hao wakushi wa Ethipia na Eritrea, kuanzia muundo na matamshi ya lugha, miili (body structure), mavazi na hata shughuli za kila siku ikiwemo hata michezo kwani Wairaqw kama walivyo waethipia wanasifika kwa riadha na wamefanana katika kila hali
Kutokana na sababu ambazo hazifahamiki japo inaaminika kuwa ni kwa sababu ya vita au njaa ya mara kwa mara inayoikumba eneo hilo la pembe ya Afrika, kundi moja la watu lilihama kuelekea kusini kufuata bonde la ufa kwa miaka mingi sana.
Walipofika kaskazini kwa Tanzania ya sasa, wakagawanyika makundi mawili ambapo kundi moja dogo lilielekea mashariki na kundi lingine likaendelea na safari yao wakifuata bonde la ufa kuelekea kusini, huku kundi hilo dogo lilifika mpaka milima ya usambara Tanga na kukaa huko mpaka leo ambao ndio wanaofahamika kama Wambugu.
Inasemekana kundi kubwa liliendelea kusonga mpaka kusini mwa Tanzania hadi Iringa wakaishi huko kwa miongo mingi sana kabla ya kuamua kurudi kaskazini, baada ya kuona eneo hilo haliwatoshi baada ya kustawi sana hapo.
Katika thesis yake ya PHD, Dr. Jackson Makwetta ambaye ni Mhehe aliandika kuwa jina la wahehe limetokana na kabila moja dogo ambalo liliishi zamani karibu na wahehe ambalo kwa sasa lipo wilayani Mbulu mkoani Arusha (sasa Manyara) ambalo wao kila wakimwona mtu asiye wa kabila lao walimwita Hee! Hee!
Lakini pia, masimulizi ya wazee wa Kiiraqw yanaanzia kwenye sehemu inayoitwa Gusir Ma/angwatay, nchi inayoelezwa kuwa ni ya baridi sana iliyopo kusini, ambapo hawakumbuki wala hakuna masimulizi yanayoeleza kabla ya kufika hapo walitoka wapi lakini wanajua baada ya kuondoka hapo wakafika sehemu inayoitwa Gusir Tiwalay yaani sehemu tuliyopigwa.
Hapa ndipo historia ya Wairaqw ilipoandikwa upya na kuchukua sura nyingine kabisa, eneo hili inasemekana ni kati ya Babati, Hanang na Kondoa. Wakiwa hapa, wairaqw walistawi sana wakiwa na ng`ombe na mazao ya kutosha, wakashamiri katika michezo na mafunzo ya kivita lakini hawakuwa na watu wa kupigana nao.
Masimulizi yanaeleza kuwa katika kipindi hiki mchezo wa kupigana kwa fimbo, yaani Ilgendi ulishamiri sana ambako kulikuwa na hadi mashindano ya kutafuta bingwa wa mchezo huo.
Vijana wakajawa na kiburi na kuona wao ni wao, wakamshinikiza kiongozi wao aliyeitwa Haymu Tippe awaletee watu wa kucheza nao (kupigana nao) na kumteka mtoto pekee wa Haymu na kumtishia kuwa kama hatawaleta watu wa kupigana nao watamuua huyo mtoto. Japo Haymu Tippe aliwaasa hasa baada ya ramli yake kuonesha madhara makubwa yatakayotokana na vita hivyo lakini vijana hao waliushikilia msimamo wao, walidai vita.
Haymu akaenda akawafuata wadatoga lakini kabla hawajafika, Haymu alitoroka na baadhi tu ya watu wa ukoo wake (Tippe) na ukoo wa Duwe na Naman (wengine wanadai ni Masaay) ambao ndio waliomsikiliza. Waliobaki nyuma na kusubiri vita walimalizwa wote na hakubaki hata mtu moja.
Katika kukimbia huko, Haymu alikuwa na mpwa wake (mtoto wa dada yake) aliyeitwa Gortoo ambapo katika kukimbia kuelekea ukingo wa bonde la ufa kwa kaskazini waligawanyika huku Gortoo akiwangoza kundi dogo kuelekea mlima Kwaraa uliopo Babati na Haymu Tippe na kundi lingine wakielekea mlima Hanang (/Anang) lakini wakaamua kukimbilia kwenye kingo za bonde la ufa eneo la Madunga na kisha kufuata kingo hizo kuelekea Kaskazini Mashariki hadi milima ya Tlahhara na Nou hadi Irqwar Daaw sehemu inayoitwa Mama Isara.
Gortoo na kundi lake wakakaa huko Kwaraa na maeneo ya Babati na ndio wakawa kabila la Gorowa au Wafyomi ambao kwa sehemu kubwa wamefanana na wairaqw isipokuwa baadhi ya matamshi ya maneno kutokana labda na mabadiliko ya mazingira lakini wanasikilizana.
Wairaqw waliishi hapo Mama Isara kwa miaka mingi sana na kuanza kuongezeka kutoka hizo koo tatu tu, wakaanza kupokea watu kutoka koo mbalimbali (assimilation) na kuunda koo mpya, mfano ukoo wa Bayo uliundwa na Wanyiramba waliofikia kwa mtu anayeitwa Bayo na kisha kuitwa Manda do Bayo! Aidha ukoo mkubwa kuliko wote wa Wairaqw ambao ni Sulle asili yao ni Wadatoga na utafiti unaonesha kuwa wadatoga wote wanaopakana na Wairaqw wanazungumza Kiiraqw na zaidi ya nusu ya hao wadatoga wanajitmbulisha kama Wairaqw tena wengi wa hao wazazi wote wawili wakiwa wadatoga.
Ziwa Gidamunyoda ambalo ni la kreta (Crater lake) limetenganishwa na barabara na Ziwa Basotu lakini ajabu ni kuwa maji yake ni ya chumvi wakati ya ziwa Basotu ni baridi (fresh) |
Je kwa nini wanaitwa Wambulu? Na Mbulu linamana gani? Endelea kufuatilia sehemu ya pili ya makala hii ya kabila hilo.
KABILA LA WANYISANZU NA NGOMA ZAO
Hawa Wanyisanzu wako zaidi mkoani Singida, kule Iramba, eneo la Kirumi linalopakana na Maswa, Meatu, Mbulu na Karatu.
Hapo walipo wanatangamana na Wasukuma, Wairaqw, Wamang’ati, Watindiga na Wasandawe. Huo ni upande wa katikati kidogo, kwa kuelekea kaskazini magharibi mwa nchi yetu. Wanyisanzu ambao ni Wabantu, si miongoni mwa makabila makubwa hapa nchini, kwa hiyo ndugu Mjadi kama hujalisikia kabila hili, usishangae. Lakini wapo na wana mambo yao ya kuvutia kuyafahamu, wao ni wakulima, mazao yao yanajumuisha ufuta, mtama na mahindi.
Lakini pia wanafuga, wanapendelea maziwa na samaki wa kukaushwa kama mboga, mfumo wao wa kuishi na kujitosheleza kwa chakula, ni kutokana na eneo walilopo, ambalo lina hali isiyotabirika kwa vipindi vya mvua na ukame. Mazingira ya hali ya hewa ya eneo lao, yamewapelekea wawe mafundi wa kutengeneza mvua. Hufanya hivyo kwa kutumia waganga na matambiko ya kuomba mvua, wakitekeleza hayo kwa kutegemea mizania ya kijinsia.
Wao wanaamini kuwa, hakuna chochote kinachoweza kuzaliwa bila jinsia, kwa hiyo, kwao, chochote kinachozalishwa lazima kitokane na jinsia mbili - ya kike na kiume. Imani hiyo si kwa viumbe hai tu, hata kwa mambo yanayotengenezwa na binadamu. Licha ya kuzingatia jinsia, lakini kuna mivutano, ambapo kama kawaida jinsia dume hutaka kuikiritimba ya kike.
Kwenye mambo ya utengenezaji mvua kwa matambiko, huchinja wanyama hususan kondoo na kutoa kafara kwa mababu, ambao hujibu kwa kuleta mvua. Matambiko, huambatana na maneno ya ibada za kijadi, lakini ili utekelezaji huo ufanikiwe, lazima kuwe na nguvu ya utatu.
Uhodari wao mwingine ni kwenye mambo ya uganga, ni kabila lenye waganga wenye uwezo mkubwa usio wa kibabaishaji. Ndugu Mjadi, kwa kifupi hayo ndiyo tuliyoyaona juma lililopita, sasa basi tuendelee mbele kutokea hapo. Ni kwamba, licha ya wale majirani niliokutajia awali wa Wanyisanzu, lakini pia zamani, Wahdazabe walikuwa majirani zao wa karibu.
Hao Wahadzabe hawakuoleana na makabila mengine, isipokuwa hawa Wanyisanzu, ambao walifika kwenye eneo hilo tangu mwanzoni mwa karne ya 18, katika kule kujitanua kwa Wabantu kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika. Wanyisanzu ndiyo wanaowafahamu vyema Wahadzabe, kuliko makabila mengine, hata watalii na wavumbuzi wengi wa mambo ya miji ya kale waliwatumia wao ili kusikilizana na hao Wahdazabe.
Kutokana na jambo hilo, kuna Wahadzabe wenye mchanganyiko wa damu na Wanyisanzu, japo kwa asilimia ndogo tu ya idadi. Ufundi wa uganga na utengenezaji wa pombe, waliutoa kwa Wanyisanzu, ambao walionekana kuwa na maarifa mengi yaliyoyavutia makabila mengine.
Kwa ujumla wao Wanyisanzu, waliambukiza utamaduni wao kwa makabila mengine yaliyowazunguka, japo eneo lao lilionekana dogo, hasa kutokana na kutangamana na makabila mengi ya jirani nao. Mathalan, hata yale mapambo ya kutoga masikio yanayopatikana kwa Wahdazabe, wameyatoa kwa Wanyisanzu.
Hata ufundi wa mambo ya uganga, waliutoa kwao, kama tulivyoona pale awali kuwa wao ni mahodari katika fani hiyo. Lakini ndugu Mjadi, lazima ufahamu kwamba, wakati huo hawa Wanyisanzu ambao ni Wabantu, walipoingia na kujitanua kwenye eneo hilo, ndipo madini ya chuma yalipoanza kutumika kutengenezea silaha.
Kwa hiyo, licha ya sasa Wabantu kuonekana ni wapole kulinganisha na watu wa mbari nyingine, lakini ni wao ambao awali walikuwa wapiganaji hodari kutokana na zana hizo mpya, kwa wakati huo. Hizo ni zama za kati ya zile za mawe na chuma, ambapo kwa walioweza kutumia zana za chuma walikuwa na nguvu kubwa ya kushinda kivita.
Kwa hiyo haishangazi kwamba, wao walikuwa katikati ya makabila mengi, huku wakiwa kabila dogo, lakini hawakuweza kugubikwa. Kwa hiyo, ushawishi ni moja kati ya mambo ambayo yaliwezesha makabila ya mbari nyingine. Kuyaiga yale ya mbari zenye nguvu kama ambavyo tohara ilivyoigwa na baadhi ya makabila jirani na Wanyisanzu. Wabantu wengi kwa asili hutahiri, tofauti na jamii za mbari nyingine.
Katika eneo lao wanalopatikana huko Kirumi, kuna michoro, japo wenyewe wanadai kutohusika nayo, lakini kwenye mapango ya mawe inakopatikana michoro hiyo, ndipo ilikuwa sehemu ya kujificha ya shujaa wa Kirumi ambaye anasemekana alikuwa Mnyisanzu. Huyo aliitwa Nyakidarama, moja kati ya watu maarufu kwenye historia ya kabila hilo.
Lakini, kwa kuwa kwenye eneo lao kuna makabila mengine pia yaliyojihusisha na michoro ya mapangoni, si ajabu kuwa hata miongoni mwao kuna ambao wanasema kuwa michoro hiyo haihusiani na kabila lao. Wanyiramba pia, ambao ni majirani zao, nao wanafahamika sana pia kwa michoro hiyo. Pia kuzungukana kwenye eneo moja kwa makabila yanayotokea mbari tofauti, ndiko ambako mara nyingi husababisha taswira tata kama ambavyo tuliwahi kuona kwa Wakamba.
Wabantu kwa asili, lakini wana taswira za makabila ya Kihamitiki. Wanyisanzu wana makundi ya koo zipatazo takriban 12, ambazo koo hizo zote huzijichukulia kuwa ndugu. Koo hizo huzalisha koo nyingine thelathini, hawa wote huunganishwa kwa kizazi cha kikeni, japo wana muelemeo wa kiumeni. Nadhani naeleweka Mjadi, tuliwahi kuona makabila yenye mfumo huo, pia kuna ile hali ya kutambuana kindugu kwa tofauti ya mbinu za utambulisho, ambao niliwahi kuzigusia hapa kwenye safu yetu.
Tuone baadhi ya hizo koo zao na koo tanzu zitokanazo na hizo, kuna Anyampanda wa Kirumi (Anyanzoka), Anyampanda wa Kinyakambi (Iyindi, Muhai au Mpilimaigulu), Anyampanda wa Anega, Anyampanda wa lgomano, Anyampanda wa Ikela, Anyampanda wa Itiili, Anyampanda wa Ikunguli, Anyampanda wa Matongo, Anyampanda wa Kinyingogo, Anyampanda wa Nyonyela, Anyampanda wa Magemelo, Anyambilu wa Gudali, Anyambilu wa Kinyankunde na Anyambilu wa Azigo.
Nyingine ni Anyambilu wa Mumba, Anyambilu wa Anyankuni, Anyankali wa Ilumba (au Iyaniko), Anyankali wa Ipilinga, Anyansuli wa Kingwele (au Mukoolo), Anyansuli wa Mukilampili (Itimbwa au Ng'wamalaga), Anyambeu, Anyambeu, Anyang'walu, Anyambwa, Anyambwa, Anyisungu, Anyambala, Asamba, Anyakumi na Anyikili.
Mjadi, koo hizo nimezitaja tu katika ule mfululizo lakini sikukutenganishia, nataraji juma lijalo nitaweza kukufafanulia. Japo mwanzoni niliahidi kuwa kwa sasa kila kabila nitalipa sehemu mbili tu, lakini kwa jinsi mambo yao ndugu zetu hawa ambayo nimeyafukua yalivyo, mtaniwia radhi, tutawapa fursa moja ya mwisho jumamosi ijayo.
Nchi ya Ihanzu, yaani mahali wanakopatikana ndugu zetu hawa, kuna misimu miwili tu, ‘kitika’ wakati wa mvua na ‘kipasu’ wakati wa ukame. Misimu hii miwili imejigawanya katika takrinban nusu mwaka kila mmoja, mvua ziko kati ya Novemba na Aprili hadi Mei.
Kipindi kinachofuata kati ya Juni na Oktoba ni ukame, hakuna mvua, mabadilishano ya vipindi vya ukame na mvua, ndiyo yanayosababisha kilimo kuwa kigumu kwenye eneo hilo. Mara nyingine mvua huweza kuja kwa wingi usiotarajiwa, na kuziondoa mbegu zilizopandwa.
Haiwezekani kulima bustani wala kilimo cha sehemu nyevu, maana kwa asili hakuna mito inayotiririka kwa mwaka mzima. Lakini wao kwa mbinu zao, wameweza kudumu na kuishi kwenye eneo lao la asili lenye hali kama hiyo niliyoitaja.
Kama ilivyo kwa jadi zote. Wanyisanzu wana ngoma ambazo huchezwa katika matukio mbalimbali ya kijamii kama harusi n.k. Ngoma kuu inajulikana kama "Nki'ninta" hii huchezwa na wanaume na wanawake rika zote. Hujipanga mistari miwili wakitizamana na wanaume huruka kwa mirindimo maalumu wanawake hutingisha mabega.
Njuga au Nkinda kwa kinyisanzu hutumika kwa kuvaliwa miguuni nazo hutoa milio pia. pia kuna mbutu ambazo hutumika zaidi kwa shughuli za dini za asili yaani wapagani. Mbutu ni bomba kama pembe ndefu ambazo hupulizwa na kutoa mlio. Wapiga mbutu waliweza kutambulika kwa kuwa midomo yao ilibadilika rangi na kuwa pink.
VYAKULA VIKUU VYA WANYISANZU
Vyakula vya asili vya Wanyisanzu ni UGALI WA NYAMA ukiambatana na mboga ya mlenda wa kusaga (Ndalu) au fresh, au mboga mbali mbali za kijani zilizokaushwa kama NSASA,NSONGA na kwa kawaida nyama hukaushwa na kuwekwa chumvi ikijulikana kama "mintanda" Vyakula hivi husindikizwa na maziwa ya mtindi.
Mlenda wa kusaga (Ndalu). |
Kwa upande wa matunda kabila hili lilitegemea zaidi matunda ambayo si kutoka bustanini ila matunda yaliojiotea yenyewe kama matogo, mbura,furu, nsalati, nkuyu, ngumo, ntundwa, lade, matini n.k. Wenyeji pia hupendelea kunywa togwa ya unga wa mtama na pombe za kienyeji.
Kipeyo au Lukulu(Kinyisanzu) ni chombo cha kunywea vinywaji mbali mbali kwa kabila la wanyisanzu. |
Hapo zamani hakukuwa na mashine za kusaga nafaka, mawe yalichongwa na kuitwa Lwala (jiwe kubwa) na dogo (Nsio) hivi vinatumika kusaga nafaka. kwa baadhi ya maeneo bado hutumia haya mawe kusaga nafaka. Nitaendelea kuelezea zaidi na kuweka taswira nitakapotembelea huko na kupewa habari zaidi.
JE! WADATOOGA NI WATU GANI?
Wadatooga au watatooga kama wanavyoitwa ni jamii ya kinailotiki wa nyanda za juu ambao wanapatikana Kaskazini mwa Tanzania hasa katika wilaya za Mbulu na Hanang mkoani Manyara japo katika miaka ya hivi karibuni wamesambaa nchi nzima ya Tanzania kusaka malisho ya mifugo yao.
Kuna aina mbili za Wanailotiki ambazo ni Wanailotiki wa Nyanda za juu yaani Highland(Southern) Nilotics ambao ni jamii za Wadatooga wa Tanzania, Dorobo na Kalenjin wa Kenya na Wanailotiki wa nyanda tambarare yaani Plains Nilotics kama Wamasai na Luo wa Kenya.
Wadatooga kama jamii |
Tabia za Wadatooga
Ni wasema kweli na hawazunguki isipokuwa kwa mambo binafsi na kabila lake huwa wasiri sana (open, honest and straight forward)
Si waoga kwa jambo lolote (ni majasiri)
Wananidhamu ya hali ya juu kwa waliowazidi umri na hasa kwa wazee, akiagizwa hakuna kubisha wala mjadala.
Kutopenda kukaa karibu na wakulima na ndiyo maana Wairaqw waliweza kumiliki maeneo ambayo yalikuwa yanakaliwa na Wadatooga kwani Mwiraqw anapojenga karibu na Mdatooga, huyo mdatooga huhama eneo hilo
Miiko ya Wadatooga
Wadatooga hawali nyama ya nguruwe (hasa ngiri pori) na nyama ya punda.
Jamii ya Barbayiga na Gisamjanga hawaoi wala kuolewa katika jamii ya Gidang`odiga (Karera) ambao ni Wadatooga wahunzi, japo wanashirikiana nao kibiashara
Mwanamke aliyeolewa ni mwiko kutaja jina la baba Mkwe wake au jina linalofanana na la mkwe wake
Mama wa Kidatooga haruhusiwi kuoga nje ya boma
Mwanamke wa kidatooga haruhusiwi kutoka nje ya boma kama hajavaa Hanang`wenda (sketi ya ngozi anayovalishwa siku anaolewa kama ishara ya pete)
Mavazi ya Wanaume
Zamani Wanaume walijifunika migorori iliyotengenezwa kwa ngozi inayoitwa "Hangda badayda" na siku hizi hufunika mashuka. Jamii ya Buradida hujifunika mashuka yenye rangi nyeusi huku barbayiga wakijifunika mashuka yenye rangi nyekundu.
Mavazi ya Kike
Wanawake walioolewa wanavaa sketi ya ngozi (hata leo hii) ambayo ni ishara ya pete inayoitwa Hanang`wenda na kwa juu (top) wanavaa "aghwada badayda" huku wasichana wakivaa "aghawada badayda" tu
Chakula cha wadatooga
Maziwa freshi ni kwa ajili ya watoto na wanaume huku wanawake na wasichana wanakunywa maziwa ya mgando Nyama: Wanaume wanakula nundu, ulimi, kidari na moyo wanawake wakila utumbo, maini na figo. Sehemu zingine wanakula wote
Damu: Wadatooga hugema damu ya ng`ombe bila kumwua ng`ombe, damu hiyo hupikwa yenyewe au wakati mwingine hupikwa kwa kuchanganywa na unga kama ugali.
Ugali: Kiasili wadatooga walikuwa hawatumii nafaka kama chakula ila siku hizi wanapika ugali wa mahindi, mtama na ulezi
Nafasi ya Mwanamke katika Jamii
Wanawake katika jamii hii hutegemewa sana hasa katika mauala ya maombi maarufu kama "ghaduweda" hasa yanapotokea majanga kama ukame, mafuriko, magonjwa ya mifugo, vifo visivyo vya kawaida au jambo lolote ambalo linahitaji "nguvu isiyo ya kibinadamu" kulitatua.
Ni mwiko kwa mwanamke kutaja jina la mkwe au hata jina linalofanana na la mkwe wake.
Pia kama wanaume wameshindwa kutatua jambo lolote katika jamii, wanawake wa kidatooga wanauwezo wa kushinikiza mpaka utatuzi upatikane.
Yapo mengi kuhusiana na makabila haya kwa leo tuishiye hapo.
No comments:
Post a Comment