Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Policarp Kardinali Pengo, amewahimiza wanawake
wakatoliki washiriki katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba yenye
kukidhi matakwa ya Watanzania.
Akizungumza hayo juzi jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa maonesho
ya miaka 40 ya wanawake wa Katoliki Tanzania (Wawata) yaliyohusisha
majimbo 34 ya kikatoliki nchini, alisema kutokana na changamoto
wazipatazo wanawake hao katika shughuli zao za ujasiliamali, ni vyema
wapewe elimu kuhusiana na ujasiliamali ili kupunguza tatizo la umaskini
nchini.
“Dunia ya leo inahitaji sana upendo, imani na ushirikiano hivyo pandeni
mbegu za upendo katika familia ili watoto waonje matunda ya mama na baba
ili wakati wa kuandaa maonyesho mengine wazingatie malezi kwa watoto na
vijana wao,” alisema Kardinali Pengo.
Pia, Pengo alisema mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake
na wajibu wake wa kikristo kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, kanisa,
jamii na taifa kwa ujumla na kuwa na maendeleo ya kiuchumi ili kukidhi
mahitaji ya familia.
Katibu Mkuu msaidizi wa Wawata Taifa, Sara Kessy, alisema changamoto
zinazowakabili ni pamoja na wengi wao kutokuwa na elimu ya biashara,
ubunifu na uzoefu, hali inayopelekea kuona ugumu wa kuendesha biashara
zao.
Maonesho hayo yaliyohudhuriwa na wageni kutoka nchi mbalimbali pamoja na
Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Francisco Padella.
No comments:
Post a Comment