Tuesday, September 25, 2012

Unahabari kwamba Sigara, pombe hatari kwa afya yako?

Tafiti za kisayansi zinazofanywa duniani kote zimeonyesha kuwa uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe, ni chanzo cha magonjwa mengi kwa binadamu ikiwa ni pamoja na saratani na magonjwa ya moyo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Marina Njelekela aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza  na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa semina ya siku 10, ya programu maalumu ya mafunzo kwa madaktari na wauguzi wanaotibu magonjwa ya moyo na saratani ya matiti.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Marina Njelekela


Alisema baadhi ya vyakula na vidonda vya tumbo ni vitu ambavyo vinasababisha saratani kwa kasi zaidi pamoja na magonjwa ya moyo, pia alitoa wito kwa Watanzania waache pombe na sigara ili kupunguza idadi ya watu wengi wanaokufa kwa saratani kila mwaka.

Programu hiyo ni mpango wa pamoja kati ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (Muhas), Hospitali ya Saratani Ocean Road na Germany Foundation, lengo lake likiwa ni ufunguzi wa kitengo cha mafunzo kinachohusiana na magonjwa ya saratani na tumbo, elimu na mafunzo kwa wauguzi na madaktari.

Katika semina hiyo, kutakuwepo na mafunzo ya vitendo ambapo Ujerumani imetoa vifaa vyenye thamani ya Sh. Milioni 7.5 na pia wanafunzi wanne kutoka Muhas ambao nao watakuwa kwenye mafunzo  hayo yanayohusisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Naye Kaimu Mkuu wa kitengo cha mafunzo ya kitengo cha tiba na magonjwa ya mfumo wa chakula Dk. John Rwegesha, alisema magonjwa yasiyoambukizi kama Malaria, kisukari, saratani, figo yanashika kasi hivyo wauguzi wanatakiwa wapewe mafunzo ya magonjwa hayo.

Profesa Rudolf Arnold kutoka Chuo Kikuu cha Ujerumani, alisema  amefurahi kuanzishwa kwa programu hiyo,  ambayo itasaidia wananchi wa EAC kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment