JK ashauriwa na Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Kufuta Chaguzi Zenye Rushwa
Kanisa
la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania limemshauri Mwenyekiti wa Taifa
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kutoa tamko la kufuta
chaguzi zote zizogubikwa na rushwa ndani ya chama hicho ili kurejesha
heshima kwa chama na serikali iliyopo madarakani.
Tamko
hilo limetolewa na Mchungaji wa kanisa hilo, William Mwamalanga, katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari kufuatia kauli ya Rais Kikwete
kwamba vitendo vya rushwa vinavyojitoleza katika chaguzi za CCM
vitakitumbukiza chama hicho kwenye shimo.
Mwamalanga
alisema rushwa ndani ya CCM imekifanya chama hicho kukosa mwelekeo
hivyo kinachotakiwa ni kwa Rais Kikwete kuchukua hatua ya kufuta matokeo
yote ya viongozi waliochaguliwa kwa rushwa ili kurejesha heshima na
imani kwa wananchi kwa chama hicho.
“Rushwa
ndani ya CCM imekuwa zaidi ya malaria, imekuwa zaidi ya ukimwi, kwa
msingi huo kauli ya Rais kukemea rushwa haitoshi,maana tatizo hili ndani
ya CCM limebaki kama ngoma isiyokuwa na wachezaji,” alisema
Mwamalanga.
Alisema
CCM ndiyo chama tawala, hivyo Watanzania walitegema kuona kinakuwa
chama cha mfano kupambana na rushwa badala yake kimekuwa kiongozi wa
rushwa hali ambayo inazorotesha upatikanaji wa maendeleo nchini.
Mwamalanga
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Kueneza Amani kwa Jamii na
dini zote nchini kama tatizo la rushwa litaachwa liendelee kushamiri
ndani ya chama hicho kikongwe, itakuwa vigumu kukemea vyama vingine vya
siasa iwapo vitachukua madaraka ya nchi.
Alisema
CCM ambayo ilitokana na Tanu ilijiwekea misingi mizuri ya kukataa
rushwa, lakini hivi sasa kimekuwa chama kinachoongoza kwa rushwa.
Kuhusu
tatizo la kuchomwa kwa makanisa, alisema serikali inapaswa kuchunguza
kwa umakini suala hilo kubaini chanzo na kwamba makanisa yote
yaliyochomwa yajengwe kwa gharama za serikali.
Rais
Kikwete akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM
(UWT), alitoa onyo kwamba vitendo vya rushwa vinavyojitokeza katika
chaguzi za ndani za CCM visipodhibitiwa, vitakitumbukiza chama hicho
kwenye shimo.
Malalamiko
ya rushwa ndani ya chaguzi za CCM yametolewa na baadhi ya wagombea wa
uenyekiti wa mikoa. Waliolalamika ni Clement Mabina (Mwanza), John
Guninita (Dar es Salaam), Thomas Ngawaiya (Kilimanjaro), Makongoro
Nyerere (Mara) na William Kusila (Dodoma).
No comments:
Post a Comment