Tuesday, October 16, 2012

Kanisa lingine lateketezwa huko Kigoma


Muumini akishuhudia Kanisa la Pentekoste (MMPT) lililopo Buronge la Manispaa ya Kigoma/Ujiji, liliteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.

Saa chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasihi viongozi na waumini wa dini za Kikiristo na Kiislamu nchini kuwa wavulilivu na kujiepusha na vitendo vya kulipiza visasi, Kanisa la la Pentekoste (MMPT) lililopo Buronge katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji limechomwa moto na kutetekezwa kabisa na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira ya saa 4:00 usiku katika eneo la Buronge mjini Kigoma.

Kashai alisema kanisa hilo lilichomwa na watu wasiojulikana na kwamba mali mbalimbali zenye thamani ya Sh. 1,337,000 ziliteketea.

Alisema  sababu za kuchomwa kwa kanisa hilo hazijafahamika na kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa huku upelelezi wa tukio hili ukiendelea ili kuwabaini wahalifu hao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

MCHUNGAJI ANENA

Mchungaji wa Kanisa hilo, Emmanuel Simon, alisema:

“Nilipata taarifa kuwa kanisa langu limeteketea kwa moto, nilikwenda Polisi Central kutoa taarifa ndipo tulikwenda eneo la tukio tukakuta kanisa lote limeteketea kwa moto.”

Alisema katika kanisa kulikuwa na mabechi 14, mlango mmoja, virago vitatu, masanduku ya sadaka na ubao wa kufundishia, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 1,337,000.

Mchungaji Simon alisema hajui watu waliochoma kanisa hilo na kuiomba serikali iangalie matukio ya uchomaji wa makanisa yanayoendelea nchi nzima.

Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa makanisa.

Alisema kanisa ni taasisi ya jamii, hivyo anaomba serikali ichangie gharama ya ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa hilo wapate sehemu ya kuabudia.

KANISA LA WAADVENTISTA LALAANI

Kanisa la Waadventista Wasabato limetoa tamko rasmi dhidi ya tukio la kuharibiwa kwa jengo la ibada la kanisa hilo lililoko Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuchomwa moto kwa makanisa mengine ya Kikristo na watu wanaodaiwa kuwa ni waumini wa Kiislamu.

Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mjini Morogoro jana, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Mashariki mwa Tanzania, Mark Malekana, alitaka serikali kulichukulia suala hilo kwa uzito wa kipekee.

Alisema licha ya kanisa hilo licha ya kupongeza kauli za viongozi wa madhehebu mengine ya dini na serikali za kukemea na kulaani viendo hivyo, lakini viongozi wa dini ya Kiislam nao wanapaswa kuwachukulia hatua za kinidhamu waumini wao wanaohatarisha amani .

“ Lazima hawa viongozi wa dini ya Kiislam wawachukulie hatua hao waumini ambao wameanza kuharibu amani ama sivyo jamii itakuwa na picha isiyo sahihi,” alisema.

Askofu huyo alisema matukio ya kushambulia na kuharibu majengo matakatifu ya ibada ya Kikristo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na hata kusababisha wasiwasi kwa waumini wa dini hiyo, jambo ambalo likiachwa liendelee linaweza kuharibu amani nchini.

“Kanisa halikufurahishwa kabisa na kitendo cha mtoto kudhalilisha kitabu kitukufu cha Kuran na nailipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua zilizochukuliwa za kumuweka kituoni mtoto huyo kwa uchunguzi zaidi na kwa usalama,” alisema.

Aliongeza: “Kitendo cha kukamatwa na polisi kinaonyesha jinsi dola isivyochukulia kirahisi mambo yayoweza kuvuruga amani miongoni mwa jamii. Kwa kweli kitendo cha mtoto huyo ni cha aibu.”

Alisema kuwa bado kanisa lake linalaani vitendo vya watu wazima wenye kujua sheria za nchi, tena watu wa kiroho kuamua kuchukua hatua mkononi kwa kuvamia kituo cha polisi na kufanya uharibifu wa makanisa ambayo hata hayakuhusika na kitendo kilichofanywa na mtoto huyo.

“Kwa kweli vitendo hivyo havikupaswa kabisa kutendwa na watu wanaomcha Mungu, kwani mcha Mungu ni mtu anayetegemewa kuwa muhimili wa amani katika jamii na kutokana na hali hiyo, ninawaomba pia viongozi wa dini ya Kiislam wawachukulie hatua za kinidhamu hawa waumini wao wanaohatarisha amani yetu ama sivyo jamii itakuwa na picha mbaya isiyo sahihi,” alifafanua Askofu Malekana.


Askofu huyo alisema kuwa kanisa lake limefarijika kwa kauli zilizotolewa na viongozi mbalimbali akiwAmo Rais Kikwete; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki; Kamanda wa Polisi Kanda na Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kwamba zinazooneshwa kukerwa na matendo hayo na kuwataka waamini wa dhehebu hilo na Watanzania kwa ujumla kuwa wavumilivu wakati serikali ikishughulikia suala hilo.

Alisema Kanisa la Waadiventista Wasabato haliwezi kutafuta haki kwa kuvunja sheria, bali linapoona kuwa halitendewi inavyostahili, huitafuta haki kwa mujibu wa sheria.

Katika vurugu zilizotokea Oktoba 12, Mbagala jijini Dar es Salaam, jumla ya makanisa saba yalichomwa moto na mengine kuharibiwa na kikundi cha watu wanaotumia kivuli cha dini ya Kiislam kufanya vurugu hizo.

MBATIA: TUJADILI MUSTAKABALI


Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi,  James Mbatia, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwakutanisha viongozi wa dini  za Kikristo na Kiislam pamoja na wanasiasa ili kujadili namna ya kumaliza chuki  inayozuka kati ya dini hizo mbili.

Mbatia alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mstakabali wa vurugu zilizojitokeza wiki iliyopita huko Mbagala, baada ya kwa waumini wa Kiislam kuchoma makanisa kufuatia kijana mmoja wa anayedaiwa kuwa Mkristo kukojolea Kuran.

Mbatia alisema tukio hilo siyo jambo la kuchukulia kibusara eti kwamba lilisababishwa na watoto, bali kutafuta ufumbuzi wa chanzo cha matatizo hayo.

“Vitendo hivi havijaibuka jana wala juzi, tumeshuhudia mara kadhaa makanisa yakichomwa hata Zanzibar tumeshuhudia, hivyo watoto nao wanajifunza kutoka kwa wakubwa kwamba chuki ipo kati ya pande hizo, tusisubiri itokee kama nchi za wenzetu kwa sababu nao walianza hivi hivi,” alisema.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, aliongeza: “Tunaiomba serikali isifumbie macho jambo hili, bali ichukue jukumu la kuwakutanisha viongozi wa dini hizo pamoja na wanasiasa kuzungunguza kwa pamoja na kuangalia namna ya kumaliza chuki iliyopo hivi sasa.”

Alisema ni jambo la kushangaza kuona viongozi wa dini na wanasiasa wamenyamaza na pasipo kusema jambo lolote kuhusiana na vurugu zinazojitokeza.

“Ni jambo la kushangaza kuona kwamba hali inazidi kuwa tete, lakini wenye kuchukua maamuzi na kukemea wamekaa kimya, ni shetani gani ameingilia nchi hii au wana lao jambo?” alihoji.

Aidha, alisema baadhi ya wanasiasa nao wamekuwa ni kichocheo cha kujenga matabaka ya udini na kwamba kitendo hicho kinatakiwa kukemewa mara moja.

 126 KORTINI LEO


Watu 126 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Dar es Salaam kufuatia vurugu zilizotokea katika eneo la Mbagala Kizuiani wiki iliyopita ambazo zilisababisha kuchoma moto makanisa na kuharibu mali.

Vurugu hizo zilisababishwa na kitendo mtoto wa miaka 14 kukojolea kurani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alisema jana kuwa askari polisi waliendelea na msako ili kubaini wahalifu katika tukio hilo, hata hivyo, alisema kuwa walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine sita juzi.

“Unajua jana asubuhi nilikuwa kwenye kikao kujadili suala hilo na kuamua kuwa muda wowote kuanzia leo (jana) watuhumiwa wote watakufikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria zitakamilika,” alisema Misime.

Watu hao wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani imedaiwa kuwa ni waumini wa dini ya Kiislam, waliovamia makanisa manne na kuyakuchoma moto, kwa madai kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 14 alikojolea kitabu cha Kurani tukufu.

Kufuatia vurugu hizo, mali mbalimbali ziliharibiwa ikiwa ni pamoja vifaa vya kuendeshea ibada, vioo vya magari vilivunjwa, hasara kamili ya uharibifu huo haijafahamika.

Rais Kikwete katika hotuba yake juzi ya kuzima mbio za Mwenge wa uhuru na Kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwataka viongozi wa dini hizo na waumini wao kuwa watulivu na wavumilivu wakati Jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi. Pia alisema wahusika wa vurugu hizo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment