Maaskofu wa makanisa ya kipentekoste Mkoa wa Arusha wameitaka serikali kuzuia baadhi ya madhehebu ya dini yanayokashifu dini nyingine hadharani ili kuendeleza amani nchini.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Maaskofu wa Makanisa hayo, Oral Sosi muda mfupi baada ya kutawazwa kuwa Askofu mteule wa Jimbo la Arusha wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God katika ibada iliyofanyika Kanisa la Betheli Kijenge.
Sosi, alisema anashangaa serikali kukaa kimya wakati viongozi wa dini nyingine wakiwatukana wao na baadhi ya viongozi wa serikali.
“Kama kweli serikali ina nia ya dhati ya kuendeleza amani katika taifa letu wachukue hatua haraka kumaliza fedheha hii dhidi ya viongozi wetu na waumini wetu tunayofanyiwa na dhehebu lingine, ”alisema Sosi.
Alisema kwa muda mrefu viongozi wao wamekuwa wakitukanwa hadharani na hata kupitia chombo kimoja cha habari hali ambayo mara kadhaa iliamsha hasira kutoka kwa vijana wao..
“Natoa dukuduku langu kwa serikali itende haki kwa kila dhehebu haiwezekani dhehebu moja kuoekana linapendelewa hasa pale inapofanya mambo yanayohatarisha amani katika jamii, ”alisema Sosi.
Alisema hali hiyo inapaswa kudhibitiwa haraka ili kuendelea kuienzi amani iliyoasisiwa na viongozi waanzilishi wa Tanzania akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Askofu huyo aliiihakikishia serikali kuwa kanisa hilo litaendelea kuwaelimisha waumini wake kutii sheria bila shuruti na kukemea vitendo vinavyokwenda kinyume na utu na maadili katika nchi.
Akitoa salamu za serikali katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema serikali inaendelea kufuatilia suala hilo na kuonya kuwa itachukua hatua dhidi ya mtu au kikundi chochote kitachoonekana kinatishai mshikamano na upendo katika jamii.
“Serikali yenu inalifahamu vyema tatizo hilo na inalifanyia kazi. Nawaomba kuwa wavumilivu hakuna mtu au kikundi chochote cha kidini kilichoko juu ya sheria ni lazima amani yetu tuilinde kwa nguvu zote, ”alisema Mulongo.
No comments:
Post a Comment