Naimani wengi mtakubaliana nami kwamba humu duniani yapo mavazi yanayotamanisha, yapo mavazi yanayomfanya mvaaji avute hisia za jinsia iliyo tofauti na yake.
Leo nitagusia suala zima la uvaaji usiofaa na nitalenga sana mavazi kwa upande wa jinsi ya kike ..Ukweli unadhihirisha kwamba Wanawake ndio wanaoongoza, katika swala hili la kuvaa mavazi yasiyokuwa ya heshima.
Ukweli ni kuwa yapo mavazi ya kike, ambayo yameshonwa kwa minajili ya kuvuta macho na kuuteka moyo wa mwanamume. Kwa minajili ya kuamsha hisia za mwanamume, Katika hali ya kawaida mavazi haya huvaliwa zaidi na wanawake wa kidunia... wale ambao bado hawajaokoka.
Na tayari mavazi haya yamejipenyeza kwenye jamii ya watu waliookoka, kiasi ambacho huwezi kuona tofauti yoyote kati ya mtu wa Mungu na mtu wa kidunia.
Ninaamini wengi wenu mtakubaliana nami kuwa, humu duniani yapo mavazi yanayotamanisha, ambayo yanayomfanya mvaaji avute hisia za jinsia iliyo tofauti na yake yake.
Iwapo uvaaji usiofaa hautadhibitiwa mapema unaweza kuwa ni sababisho la uzinzi wa kutisha ndani ya jamii ya wateule wa Mungu, ndani ya makanisa yetu kwani uvaaji huo unaweza kushusha kabisa heshima ya jamii ya watu waliookoka.
Nia yangu sio kukulaumu wewe ambaye aidha kwa kutokujua au kwa kutojali, umejikuta tayari umeshapitiliza mipaka kwa kuvaa mavazi yasiyofaa. Nia yangu ni kukumbusha kuwa ipo haja ya kuwa makini na uvaaji wako.
Kwani Mungu anajali sana jinsi tunavyovaa na kwamba ameeleza bayana kupitia neno lake, ni jinsi gani wanadamu wanapaswa kuvaa. Kama utavuka mipaka ya aina ya uvaaji uliowekwa na Mungu, utahukumiwa naye kwani hili halina ubishi.
Uvaaji usiozingatia maagizo ya Mungu ni hatari sana kwa kanisa, hiyo ni kama kijinga cha moto ndani ya msitu mkubwa, ambacho kinaweza kuteketeza msitu wote iwapo hakitazimwa mapema.
Na Biblia inatuonya katika 1Wakorintho 5:6 kwa kutuhoji iwapo hatujui kuwa ‘chachu kidogo hulichachua donge zima?’ Maneno haya yalizungumzwa na mtume Paulo baada ya wateule waliokuwa katika mji wa Korintho kujisahau mno mpaka zinaa ya kutisha ikaingia katikati yao. Yaani mpaka ikafikia hatua ya mshirika kumwoa mke wa baba yake mzazi.
Pale kanisa linapojisahau matatizo kama haya yaliyojitokeza kati ya wateule waliokuwa Korintho, yanaweza vile vile kujitokeza katika kanisa la leo na ndio maana nikasema ipo haja ya kupambana na tatizo la mavazi yasiyofaa mapema kabla hali haijawa mbaya. Binafsi ninaamini hatujachelewa, bado hali inaweza kurekebishwa.
Uvaaji hu usipodhibitiwa, unaweza kuenea makanisani mwetu na kuyateketeza. Na ukweli ni kuwa hatari hii haipo mbali sana. Tayari imeshabisha hodi katika baadhi ya makanisa. Kwa makanisa mengine hatari hiyo imeshajikita kabisa na hali inatisha.
Nakumbuka tatizo la kuvaa mavazi yasiyo ya heshima lilianza kidogo kwa kuwahusisha washirika wachache tu, tena wakiwa wanavaa nguo ambazo hazikuwa mbaya sana. Lakini kidogo kidogo tatizo likakua kwa wavaaji wa aibu kuongezeka.
Vile vile mavazi yenyewe yakaongezeka katika ubaya wake, yaani yakaongezeka katika ile hali ya kumwacha mtu kuvaa mavazi yasiyokuwa na maadili
Baadhi ya makanisa leo hii wadada na wamama wamekuwa wakivaa mavazi ya aibu yanayowaacha mapaja, viongo vya mwili kuachwa wazi au migongo yao wazi kabisa.
Miaka ya nyuma kidogo wakati mtindo wa vazi la mpasuo ulipoingia nchini mwetu, mwanzoni wanawake wacha Mungu hawakuiga mtindo huu. Hata wahubiri na waimbaji wa nyimbo za Injili walionya sana juu ya mipasuo ya aibu.
Lakini baada ya muda, wakaanza kujitokeza waumini wachache waliodiriki kupasua magauni au sketi zao, tena walianza kwa kampasuo kadogo tu, ambako eti sio kakubwa sana na kwamba hakana neno.
Baada ya muda mfupi tu wavaaji wa mipasuo midogo wakaongezeka., siku zilipozidi kwenda ikaja mipasuo mikubwa yenyewe ukaongezeka, sambamba na wavaaji wake.
Leo hii ni jambo la kawaida kabisa kuwakuta mabinti pamoja na wamama wengi tu wakiwa wamevalia mipasuo ya aibu makanisani mwao; tena bila wasiwasi wowote.
Siku hizi uvaaji wa mipasuo ya aibu umezoeleka mno makanisani, kiasi ambacho nguo hizi zinaonekana kama vile ni vazi la kawaida kabisa lisilo na tatizo lolote. Ndio maana nikasema kuwa katika baadhi ya makanisa hali inatisha, na ukweli ni kwamba hali hii imezidi kukuwa kwa sababu tatizo halithibitiwi/halikuthibitiwa tangu mwanzo.
Halikushughulikiwa kikamilifu pale lilipoanza kujitokeza. Kwa sasa tayari limeshajikita makanisani na ndiyo maana watu wachache wanapojitokeza leo kukemea hali hii, wanaonekana kama wendawazimu, wanaonekana kama waliopitwa na wakati au washamba wa kutupwa.
Hata kwa upande wa jinsi ya kiume (mwanamume) wengi wao wamekuwa wakivaa mavazi ya ajabu mbele ya jamii iwazungukayo..unakuta mwanaume anavaa suruali na kuishusha chini makalio yake eti wanasema ni 'KATA K ' eti wanakwenda na wakati.
Mbali na hilo wengine wamekuwa wakivaa mavazi ya kubana, yanayouchonga mwili wao eti ni kwenda na wakati...tumekuwa tukiiga vitu ambavyo si tamaduni zetu za Kiafrika na kuiga tamaduni za watu wengine kwani hiyo inapelekea hata vile vizazi vijavyo huiga tabia watakazo zikuta kwenye jamii yetu.
Ni kwa nini kizazi cha leo kina tabia ya kuvaa mavazi yasiyositiri miili yao vizuri? Ni kwanini wazazi wanavaa mavazi mabaya mbele ya watoto wao na watoto watoto huvaa mavazi mabaya mbele ya wazazi wao?
Dawa ya tatizo ni kulishughulikia mapema na tunatakiwa tupambane nalo kabla halijakomaa na kuwa sugu. na siyo kuliacha likue na kuzoeleka kama vile sio tatizo tena.
Ndio maana Biblia inatuagiza kuwa, “Basi, jisafisheni mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu” (1Wakorintho 5:7). Kanisa linatakiwa lijisafishe,lijirekebishe. Mavazi yote yasiyofaa yanatakiwa yaondoke katikati ya kusanyiko la watu wa Mungu.
No comments:
Post a Comment