Askofu wa Kanisa la Kianglikana
nchini, Dk. Valentine Mokiwa, amewataka watendaji wa kanisa hilo kuwa
macho na baadhi ya watu wenye uwezo mkubwa kifedha kupandikiza chuki
ndani ya madhehebu hayo.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,
mjini hapa wakati wa ibada ya shukrani baada ya kumalizika kwa mgogoro
uliokuwa unaikumba kanisa hilo, Dk. Mokiwa alisema imeibuka tabia kwa
baadhi ya viongozi wa kanisa kuogopa kuwakemea watu wenye uwezo mkubwa
kifedha hata kama wanakiuka sheria za kanisa.
Aidha, kiongozi huyo pia amewataka watendaji wa kanisa hilo
kutokubali kupokea fedha za muumini yeyote zitakazobainika kuwa
hazikupatikana kihalali.
“Ni vyema kutafuta fedha kwa bidii ili kupambana na umaskini na sio
dhambi mtu kuwa fedha nyingi lakini ni dhambi kutafuta fedha kwa njia
zisizo halali na ni vibaya zaidi kutumia fedha hizo kupandikiza chuki
mahali popote ikiwemo ndani ya kanisa” alisema askofu Mokiwa na
kuongeza:
“Itakuwa dhambi kubwa kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuwatetemekea
na kuwaweka mbele watu wenye fedha na kushindwa kuwakemea pale
wanapokwenda kinyume na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maelekezo
ya kanisa na maelekezo ya Mungu.”
Askofu Mokiwa pia amewaonya waumini wanaodhani kuwa kwa kutumia fedha
zao watapata nafasi ya kuyavuruga madhehebu ya dini na kuwataka
viongozi wa madhehebu ya dini kuwa macho na makundi ya watu wa
aina hiyo ambayo amedai yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.
Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu wa Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro
Stanele Hotay, pamoja na kuwashukuru waumini wa kanisa hilo kwa
mshikamano walioonyesha wakati wote wa mgogoro, aliwawataka kuendeleza
msimamo huo.
Aidha, Askofu huyo ameiomba serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu
na viongozi wa madhehebu ya dini katika nyanja mbalimbali zikiwemo za
kiuchumi na kukabiliana na umaskini unaoendelea kuikabili jamii.
Wakiwasilisha salam za serikali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, walisema
serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa madhehebu ya dini na
kuhakikisha kuwa uhuru wa kuabudu unadumishwa kwa mwananchi wote.
Dk. Nchimbi amewataka waumini wa madhehebu ya dini wanaopambana na
viongozi wao kuacha mara moja utaratibu huo kwani licha ya kuwa
hauna tija utawasababishia kupata laana toka kwa Mungu.
No comments:
Post a Comment