Kadhalika, wametakiwa kuiga mfano wa Mwalimu Nyerere ambaye wakati wa uongozi wake, hakunyanyasa watu na alitaifisha hata shule zilizokuwa zinamilikiwa na Kanisa Katoliki ili watu wote wapate elimu sawa na kuwa wamoja bila kujali dini, itikadi, rangi wala kabila.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirika la Farijika, Familia na Jamii Afrika Mashariki, Padre Baptiste Mapunda, wakati akiongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki Parokia ya Manzese, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Farijika, Familia na Jamii Afrika Mashariki, Padre Baptiste Mapunda |
Padri Mapunda alisema Nyerere, aliwaokoa Watanzania kutoka kwenye utumwa wa wakoloni na mabepari na alikuwa na unyeyekevu kama Musa alivyowaokoa Waisrael kutoka utumwani.
“Mwalimu Nyerere ni kama nabii, dunia nzima inaheshimu uongozi wake, alisisitiza watu wote kuepuka chuki na wivu na aliongoza kwa kutumia Azimio la Arusha, lakini sasa wajanja wachache wameliondoa azimio hilo na kukumbatia rushwa na ufisadi,” alisema katika mahubiri yake.
Aliongeza kuwa matajiri na mabepari wamevamia nchi kwa kujiita wawekezaji huku wazawa wakiishia kuwa maskini kwa sababu ya viongozi wachache wanaokula rushwa na kuangamiza walio wengi.
“Miaka 50 hakuna kilichofanyika zaidi ya kupoteza fedha huku wananchi wakililia huduma mbalimbali za kijamii. Kwa nini fedha hizo zisitolewe kwenye shule na hospitali ili watu waone serikali yao inawajali?,” Alihoji huku akishangiliwa na waumini waliohudhuria ibada hiyo.
Akizungumzia utoaji wa maoni kwenye mchakato wa Katiba mpya, Padri Mapunda, alisema kuna haja ya wananchi kupata Katiba mpya itakayoainisha matumizi ya rasilimali zilizopo nchini.
“Tunatakiwa kujua matumizi ya rasilimali zetu, maliasili, mikataba mibovu inayobomoa uchumi wa nchi yetu isifumbiwe macho vyote vianishwe kwenye Katiba mpya,” alisema na kuongeza:
“Wananchi wasiache kujitokeza kutoa maoni yao kwa kuwa hali sasa imekuwa siyo shwari hata uhuru wa habari hakuna, viongozi wachache wanakumbatia utumwa na kusahau uzalendo wao,” alisema.
Akifafanua zaidi, Padri Mapunda alisema maombi yanahitajika katika kipindi hiki cha kutoa maoni ya Katiba hiyo ili nchi ipate viongozi wanaojali bila kutanguliza fedha mbele na nchi irejee kama wakati wa hayati Mwalimu Nyerere.
No comments:
Post a Comment