Monday, August 20, 2012

Wengi wasema hawataki vita na Malawi



Hatua ya Rais Jakaya Kikwete, kutangaza rasmi kuwa Tanzania haina mpango wala nia ya kuingia katika vita na nchi jirani ya Malawi imepongezwa na wanasiasa na wasomi ambao sasa amewageukia kwa kuwakosoa viongozi waliotoa kauli zilizoonekana kuhamasisha vita.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti wakati wakitoa maoni yao kuhusiana na mgogoro kati ya Tanzania na Malawi unaotokana na tofauti zao kuhusu mpaka katika Ziwa Nyasa, walisema kauli ya Rais imewapa faraja kubwa Watanzania ambao hawapendi kuona nchi yao ikiingia katika vita.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mjini Maputo, Msumbiji alipokutana na Rais Joyce Banda wa Malawi wakati wa mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

MZIRAY WA APPT MAENDELEO

Mwenyekiti wa APPT Maendeleo, Peter Mziray, alisema kama kuna jambo ambalo Rais Kikwete anapaswa kupongezwa na kila Mtanzania mpenda amani ni kukataa Tanzania kuingia katika vita na Malawi kwani kuna athari kubwa ambazo nchi inaweza kupata.

“Tunasikitishwa na kauli za baadhi ya viongozi waliokuwa wakitoa kauli zinazoashiria kuhamasisha vita kwani huu siyo muda mwafaka na pia ni aibu kutaka kupigana na Malawi ambao ni jirani zetu ambao tunahirikiana nao katika mambo mengi, “ alisema Mziray.

Mziray alisema bila shaka kauli zilizotolewa na viongozi kadhaa kuhusu mgogoro huo walikuwa wanajitafutia umaarufu kwani haukuwa muda mwafaka kwa Tanzania kujigamba kuwa tuna jeshi zuri na hivyo tupo tayari kupigana vita.

MBATIA WA NCCR-MAGEUZI

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema hatua ya Rais Kikwete kutaka diplomasia itumike katika kufikia mwafaka ni jambo linalopaswa kupongezwa na Watanzania.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, alisema kauli za baadhi ya viongozi ndani ya serikali zilikuwa zinatolewa kushabikia vita na kwamba hali hii imeonyesha suala la uwajibikaji wa pamoja ndani ya serikali linatakiwa kuzingatiwa.

“Tunamuunga mkono Rais Kikwete kwa kauli yake ya busara ya kukataa nchi yetu isiingie katika vita, kwani yapo matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi kuliko kuingia kwenye vita,” alisema Mbatia.

DK. SLAA WA CHADEMA


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema kauli zinazotofautia zilizotolewa na viongozi wandamizi wa serikali katika sakata hili zimeonyesha ni jinsi gani serikali ilivyoparaganyika.

“Katika suala la mgogoro huu Rais anapopingana na kauli za mawaziri wake ni dhahili kuwa nchi imekosa dira na mwelekeo hivyo bado tuna kazi kubwa,” alisema.

Dk. Slaa alisema gazeti moja la Malawi limemnukuu Rais Kikwete akidai kuwa wanasiasa waliotoa kauli hizo ambao ni wapinzani ni helehele na kwamba kama ni kweli alisema hayo nalo ni tatizo na ni dalili kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekosa dira.

MREMA WA TLP

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema chama chake kinamuunga mkono Rais Kikwete kwani hakuna sababu za Tanzania kuingia katika vita na Malawi ambao ni marafiki zetu.

Mrema alisema hakuna sababu yeyote kwa Tanzania kuingia katika vita na Malawi na kwamba hakukuwa na haja kwa viongozi  kujigamba kuwa tuna jeshi zuri wakati hatufahamu nani yupo nyuma ya Malawi kumsaidia.

PROFESA BAREGU

Naye Mhadhiri Mwandimizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) cha jijini Mwanza, Profesa Mwesiga Baregu, alisema matamko yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje ya Bunge, Edward Lowassa, kuwa Tanzania iko tayari kuingia vitani ikibidi, hayakuwa ya kidiplomasia.

Alisema hakuona sababu ya Membe na Lowassa kutoa matamshi ya vitisho badala ya kujikita kwenye muelekeo wa kidiplomasia kwa kuwa tatizo la mpaka kati ya Tanzania na Malawi ni la siku nyingi na kwa nyakati tofauti limekuwa likiibuka na kuzimika.

Alisema safari hii suala limejitokeza kwa sura tofauti na hivyo la muhimu ni kujiuliza kwa nini limeibuka kwa namna lilivyoibuka na akashauri kwamba, la msingi ni kulifanyia kazi ili limalizike kabisa.

“Ni vizuri Rais ameweka wazi kama Amiri Jeshi Mkuu kuwa Tanzania haina mpango wa kupigana na Malawi ila itatumia njia za kidiplomasia kulishughulikia suala hili. Lakini sehemu ambayo ninaona alikengeuka ni pale alipoacha kuweka wazi msimamo wetu kama alivyofanya Rais mwenzake (Banda) pale aliposema kwamba Malawi inalimiliki ziwa hilo kwa asilimia 100. Ilibidi na yeye aweke msimamo wetu kwamba sisi tunamiliki ziwa hilo kwa aslimia 50,” alisema.

Profesa Baregu alisema kuweka msimamo wetu wazi wazi kama alivyofanya Rais Banda ni kitu muhimu ambacho hata ile kamati ya wataalamu wataoshughulikia mazungumzo hayo wangeenda nayo kifua mbele badala ya kuingia kama wanyonge.

Baregu aliongeza kuwa hata Jumuiya ya Kimataifa nayo ingeelewa wazi wazi kuwa Watanzania wanadai nini kwenye ziwa hilo.

Alisema njia ya mazungumzo italimaliza suala hili, ukichukulia ukweli kwamba kuna vyombo vingi ambavyo vinaweza vikasaidia kutatua mgogoro huu, ukianzia na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo za Kusini mwa Afrika pamoja na wale walioweka mipaka hii, kwa maana ya Waingereza na Wajerumani.

DK. BENSON BANA

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Rais Kikwete juu ya kadhia ya mpaka ni ya kupongeza na inaonyesha hulka aliyonayo Rais na Watanzania kwa ujumla wake.

Alisema kwa kawaida Watanzania wana hulka ya upore na si wagomvi mpaka pale wanapokuwa wamechokozwa ndipo wanapoonyesha makucha yao.

Aidha, Dk. Bana alisema hata matamshi ya Rais Banda nayo yanaonyesha jinsi alivyo muungwana na kitendo chake cha kukutana na Rais Kikwete na wakazungumza kwa amani ni cha kupongezwa.

Alisema kauli iliyotolewa na Lowassa inaonyesha muelekeo mzima wa Bunge ambao wao kama wasomi wamekuwa wakiupinga kwa muda mrefu mhimili huo wa dola kuonekana kuingilia kazi za mihimili mingine.

“Kazi ya Bunge pamoja na nyingine ilizonazo ni kuisimamia na kuishauri serikali na si kufanya maamuzi ya kuiingiza nchi vitani. Anayetoa amri ya kuiingiza nchi vitani ni Amiri Jeshi Mkuu, ambaye ni serikali na si Bunge, Bunge huwa linataarifiwa kwa ajili ya kuridhia na si vinginevyo,” alisema.

Alisema njia ya mazungumzo ni mwafaka kati ya nchi hizi mbili kwa kuwa kama kwa miaka yote 50 zimeweza kuishi kwa amani, basi hakuna kitu cha kuzifanya sasa hivi zikaingia vitani ili kutatua  mgogoro badala ya mazungumzo.

DK. AZAVELI LWAITAMA

Naye Dk. Azaveli Lwaitama, Mhadhiri mstaafu Filosofia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kwamba Tanzania na Malawi hazina sababu ya kupigana vita kutokana na mipaka iliyowekwa na wazungu ambayo ilitenganisha ndugu wanaotoka katika ukoo mmoja na kuwaweka katika nchi mbili tofauti.

Alisema kwamba alichoongea Rais Kikwete ni cha kupongeza kwa kuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu na kwamba vita ya kupigania mipaka kwa sasa hivi haina tija na hasa kwenye nchi maskini kama za kwetu.

“Siwalaumu Membe na Lowassa kwa kuwa walizungumzia possibilities (uwezekano), lakini sasa maadam Rais ameshasema, basi jambo hili limekwisha” alisema.

MTATIRO WA CUF

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Julius Mtatiro, alisema chama chake kinampongeza Rais Kikwete kwa kutaka amani kuliko vita ambavyo vingeweza kusababisha nchi kuathirika kiuchumi kama ilivyokuwa wakati wa vita dhidi ya nduli Iddi Amin wa Uganda.

CHANZO CHA MGOGORO

Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, hivi karibuni bungeni alitoa tamko la serikali kuhusu mzozo wa mpaka huo na kuitaka Malawi kusitisha shughuli zote za utafutaji wa mafuta na gesi katika ziwa hilo hadi mzozo huo utakapopatiwa ufumbuzi.

Pia ilielezwa kwamba Tanzania ilikuwa na uwezo wa kulinda mipaka yake na haiwezi kuruhusu sehemu ya taifa hilo kukaliwa na nchi nyngine yoyote.

Kabla ya tamko la Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akikaimu nafasi ya Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Samuel Sitta, alisema vitendo vinavofaywa na Malawi kwa kutoa leseni kutafiti gesi na mafuta katika eneo la Tanzania ziwani humo, hakikubaliki na kwamba nchi ilikuwa tayari kwa lolote katika kulinda mipaka yake.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walikuwa wamepata taarifa kutoka kwa viongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa walikuwa wamejiandaa kwa njia zote kulinda mipaka ya nchi.

 

No comments:

Post a Comment