Wenyeji wa Mkoa wa Mbeya wanaoishi
jijini Dar es Salaam wamewasilisha barua na vielelezo katika ofisi ya
Mamlaka ya Taifa ya Utambuzi (Nida) kupinga Askofu Mkuu wa Kanisa la
House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship, Mulilege Mkombo,
anayedaiwa kujiandikisha kama mzaliwa wa Tanzania kwa lengo la kupata
kitambulisho cha Taifa.
Katika barua hiyo ambayo imepelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Nida,
Dickison Maimu, na nakala kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na
Usalama, Edward Lowassa, wameeleza kuwa Askofu Mkombo jina lake halisi
ni Mukombo Muyodi aliyezaliwa Aprili 4, mwaka 1964 eneo la Butumba
Kimakondolo Lumbumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Imeeleza kuwa askofu huyo katika mchakato wa kupata kitambulisho cha
uraia kwa jina la Mulilege Mkombo, amejiandikisha katika Kata ya Boko
Magengeni jijini Dar es Salaam kama raia wa Tanzania.
Maimu akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki alithibitisha kupokea
barua na vielelezo kutoka kwa wananchi hao vya pingamizi dhidi ya askofu
huyo na kwamba mamlaka yake kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji
vimeanza uchunguzi wa suala hilo.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyoandikwa na kusainiwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa taasisi inayoshughulikia uhifadhi wa mazingira na Idara ya
Haki za Binadamu (MRECA), William Mwamalanga, ambayo NIPASHE imefanikiwa
kuona nakala yake, imeeleza kuwa askofu huyo siyo mzaliwa wa Tanzania
bali amezaiwa DRC.
“Timu yetu ya watafiti imefanya kazi na kubaini pasipo shaka kuwa mtajwa
hapo juu ni raia wa DRC hasa baada ya kumuhoji mkewe aitwaye Mary
Mukombo ambaye walifunga ndoa yao huko huko DRC na wazazi wao walihusika
kufunga ndoa hiyo na kutambuliwa na mamlaka ya DRC,” inaeleza barua
hiyo.
Barua hiyo imezidi kueleza kuwa watafiti wa MRECA wamebaini vyeti vya
taaluma na viapo vya kisheria kutoka mamlaka ya DRC na kwamba Askofu
Mukombo Muyodi alifanikiwa kughushi vyeti vya kuzaliwa baada ya kununua
wazazi mkoani Mbeya na kujiita Mulilege Mukombo Kameka jina ambalo ni
maarufu kwa kabila la Wanyakyusa mkoani humo.
“Ikumbukwe ni vigumu kujua nia ya Mukombo Muyodi kununua wazazi na
kujipachika jina la Mulilege Mkombo na kumfukuza mkewe huku akitajwa
kuwa alikuwa askari wa zamani wa DRC,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, taasisi hiyo ya MRECA imewasilisha Nida vyeti vya kuzaliwa vya
askofu huyo akiwa DRC, vyeti vinavyodaiwa vya kughushi na pasipoti ya
kusafiria hapa nchini.
Mara kadhaa NIPASHE ilimtafuta askofu huyo bila mafanikio, lakini mkewe,
Greener Pulin, alizungumza kwa niaba ya mumewe akizungumza na kusema
kuwa watu wanaohoji uraia wa askofu baadhi ni waumini wa kanisa hilo
ambao wanatumiwa na baadhi ya watu kwa lengo la kumdhoofisa katika
utendaji wake wa kazi.
No comments:
Post a Comment