Wednesday, September 5, 2012
Mabaki ya mwili wa Rugambwa kuzikwa upya Oktoba
Mwili wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, unatarajiwa kufukuliwa na kuzikwa upya katika Kanisa Katoliki mjini Bukoba mwezi ujao.
Kardinali Rugambwa alifariki dunia Desemba mwaka 1997 na alizikwa katika Kanisa dogo la kwanza Katoliki Kashozi Bukoba mwaka huo huo.
Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa shughuli za kufukua mwili huo zitafanyika Oktoba, 6 mwaka huu.
Alisema shughuli hizo zitaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Kardinali Rugambwa. Askofu Kilaini aliwaomba Watanzania wengi wajitokeze katika shughuli ya kufukua mwili huo na kufanya mazishi mapya na kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake.
Alisema wageni mbalimbali mashuhuri wamealikwa akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya tatu Benjamin MKapa, mabalozi na wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Alisema katika kumuenzi, wameamua kuanzisha mfuko wa elimu wa Rugambwa kwa ajili ya kuendeleza harakati za kukuza elimu kama alivyofanya wakati wa uhai wake.
Kardinali Rugambwa ni Mwafrika wa kwanza kushika daraja hilo la kiroho na ni moja wa viongozi wa kidini waliokubaliwa na kuheshimiwa duniani.
Alizaliwa kijiji cha Bukongo, Parokia ya Rutabo, Kata ya Kamachunu, wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera Julai 12, 1912, akitokea katika familia iliyotukuka, familia ya kitawala.
Alipata elimu yake ya Sekondari katika shule ya Seminari ya Rubya Junior na kisha kujiunga na Semiri Kuu ya Katigondo nchini Uganda ambako alihitimu masomo ya Falsafa na Theolojia Desemba 12, 1943.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment