Thursday, October 18, 2012

MAOMBI NI NINI?


"Tufundishe Jinsi Ya Kuomba."

Je, umewahi kugundua kwamba wakati unapoamua kuomba unapata upinzani kutoka kwa ulimwengu, ukishirikiana na mwili wako, pamoja na Shetani? Unakuwa hutulii, unapata njaa, au usingizi, au unaanza kuwazia mambo mengine mengi unayolazimika kuyafanya.

1. Maombi Ni Nini?

Maombi ni mambo mengi kwa watu wengi. Ni mambo mengi kuanzia mazungumzo hadi kazi za mikono na za kiroho. Katika Lk 11:9,10 kuna ngazi tatu za maombi, nazo ni:

Ngazi Ya Kwanza Ni Rahisi Sana - Omba.
Omba – utakalo, ingawa Baba yako anajua hitaji lako hata kabla hujamwambia. Uwe kama watoto wadogo ambao ni mabingwa wa kuomba! Soma 2 Sam 5:17-25 ili uone namna Daudi alivyogundua jambo la kufanya kwa kumwuliza Mungu. Kufahamu mawazo ya Mungu kutakuongoza hatua kwa hatua kuelekea kwenye usalama mkuu (1 Yoh 3:21). Kwa upande mwingine soma kitabu cha Yoshua mlango wa 9 na hasa ule mstari wa 14 ili uone upumbavu wa kutokumwomba Bwana.

Ngazi Ya Pili Ni Nzuri Kwelikweli – Tafuta.

Kwa ufupi ni kumtafuta Yesu, kwa kuzingatia yeye ni nani. Furahia kutumia muda mrefu pamoja Naye, ukimwambia kila kitu, ukimsikiliza, bila kumletea mlolongo mrefu wa mahitaji.

Ngazi Ya Tatu Huubadilisha Ulimwengu – Bisha.

Bisha – mlangoni kwa mkuu wa Kanisa; nawe utamsikia Yesu akisema, “Ingia”. Anakualika wewe na waamini wengine kwenye maombi kwa sababu Yeye mwenyewe ni mwana maombezi, akiomba kwa ajili ya ulimwengu wa watu waliopotea. Kujiunga naye katika maombi kunaleta maombezi ya kwelikweli, yanayoweza kuchukua masaa au hata siku kadhaa (Ebr 7:24,25).

2. Ya Nini Kuomba?


Zipo sababu nyingi za kuomba, ambako ni mawasiliano ya njia mbili kati yako na Baba yako kadiri ukuavyo. Hata hivyo kulingana na ufahamu aliotupa Yesu katika Lk 11:21 tunazo sababu nzuri sana za kuomba:

    Yule mtu mwenye nguvu anamwakilisha Shetani.
    Nyumba yake ni dunia, na vitu vyake vinavyolindwa ni watu.
    Yule mwenye nguvu zaidi ni Yesu.
    Sisi tuko ndani yake na tumeketishwa pamoja naye (Efe 1:23) (Efe 2:6).
    Nyara ni watu wote wanaookolewa kupitia maombi; familia yako, jirani zako, na hata watu wengine walioko mbali.

3. Ni Nani Aombe?
Katika Lk 18:1, Yesu anawaambia wafuasi wake, waume kwa wake, wavulana kwa wasichana, vijana kwa wazee, kwamba wanapaswa kuomba kila wakati bila kukata tamaa. Maombi ni huduma yenye nguvu na iliyo wazi kwa kila mwamini, awe kijana au mzee.

4. Tuombe Tukiwa Wapi?

Katika nyakati za Biblia watu walisafiri ili wakafanyie maombi yao ndani ya Hekalu au katika maeneo mengine ya Kiyahudi ya kukusanyikia. Biblia inasema kwamba leo mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu, kwahiyo unaweza kuomba mahali po pote, wakati wo wote, na kwa namna yo yote: ukiwa umepiga magoti, ukiwa unatembea, ukiwa unafanya kazi, ukiwa umekaa, na hata ukiwa umelala chini.

5. Je, Tuombe Wakati Gani?
Yesu anasema tuombe  ‘kila mara,’ na Paulo anasema, ‘nyakati zote’. Iwe mchana au usiku, wakati wote kama nidhamu inavyodai, au kama moyo unavyoelekeza, tunaweza kuomba. Yesu anasema tuwe wavumilivu katika maombi, na Paulo anasema tuombe katika Roho kwa sala zote na maombi, ikiwa ni katika ukimya au katika msisimko mkubwa.

6. Je, Tuombe Namna Gani?

Katika Lk 11:2-4 Yesu alitufundisha namna ya kuomba. Haina maana kwamba turudie maneno hayo kila mara bila kufikiri au bila upendo kama ilivyo kwa baadhi ya makanisa, lakini ni lazima yaombwe kutoka moyoni na akilini pia.

Anza Kwa Kuzungumza Na Baba Yetu

Tukumbuke kwamba Baba yetu ni Baba aliye mkamilifu katika kutupenda na kututunza, si kama walivyo mababa wengi wa kidunia.

Litukuze Na Kulibariki Jina Lake

Chukua muda kumwabudu na kumshukuru kabla hujasema lo lote. Mwambie Mungu jinsi unavyompenda na umshukuru kwa upendo wake kwako, kwa familia yako, na kwa taifa lako (Yn 4:23).

Omba Kwamba Ufalme Wake Uje

Ufalme ni pale mfalme anakotawala,  kwahiyo mwombe Mungu kwamba Ufalme wake uje pale unakohitajika; katika maisha yako, katika familia yako, na katika taifa lako.

Omba Mapenzi Yake Yatimizwe

Kinyume na matukio maovu katika jamii.

Omba Mkate Wako Wa Kila Siku

Baba yuko radhi kutupatia mkate.

Mwombe Mungu Akusamehe Dhambi Zako

Acha damu ya Yesu itakase kila dhambi.

Na Kwa Kuwa Sasa Umesamehewa
Kusamehe wengine ndilo sharti la sisi kupokea msamaha wetu.

Uongozi Wa Mungu

Mwombe Mungu akuongoze maishani.

Mwombe Mungu Akuokoe Na Uovu

Uliojificha ndani yako, katika familia yako, na ndani ya vitu kama madawa ya kulevya na vita.

Mtukuze Kwa Ufalme Wake Na Utukufu

Hii ni fursa nyingine ya kuabudu, kusifu, na kutamka maneno ya imani. Ona jinsi muda unavyopita haraka unapoomba namna hii.

Hatimaye hapa pana siri ya maombi yenye nguvu. Yesu anahitimisha somo lake kuhusu maombi katika Lk 11:13 kwa kutuambia ni jinsi gani Baba alivyo radhi kutupatia Roho Mtakatifu. Kwahiyo kila mara mkaribishe Roho Mtakatifu aongoze  maombi, unapokuwa peke yako au kwenye kikundi, halafu uone jinsi atakavyokuwezesha kuomba vizuri. Masaa mengi yatapita kama dakika chache tu (Lk 11:5-8) (Efe 6:18).

 Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili

No comments:

Post a Comment