|
Muumini
akishuhudia Kanisa la Pentekoste (MMPT) lililopo Buronge la Manispaa ya
Kigoma/Ujiji, liliteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana usiku wa
kuamkia jana. |
Saa chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasihi viongozi na waumini
wa dini za Kikiristo na Kiislamu nchini kuwa wavulilivu na kujiepusha
na vitendo vya kulipiza visasi, Kanisa la la Pentekoste (MMPT) lililopo
Buronge katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji limechomwa moto na kutetekezwa
kabisa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma,
Frasser Kashai, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira
ya saa 4:00 usiku katika eneo la Buronge mjini Kigoma.
Kashai
alisema kanisa hilo lilichomwa na watu wasiojulikana na kwamba mali
mbalimbali zenye thamani ya Sh. 1,337,000 ziliteketea.
Alisema
sababu za kuchomwa kwa kanisa hilo hazijafahamika na kwamba hakuna mtu
aliyejeruhiwa huku upelelezi wa tukio hili ukiendelea ili kuwabaini
wahalifu hao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
MCHUNGAJI ANENAMchungaji wa Kanisa hilo, Emmanuel Simon, alisema:
“Nilipata
taarifa kuwa kanisa langu limeteketea kwa moto, nilikwenda Polisi
Central kutoa taarifa ndipo tulikwenda eneo la tukio tukakuta kanisa
lote limeteketea kwa moto.”
Alisema katika kanisa kulikuwa na
mabechi 14, mlango mmoja, virago vitatu, masanduku ya sadaka na ubao wa
kufundishia, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 1,337,000.
Mchungaji
Simon alisema hajui watu waliochoma kanisa hilo na kuiomba serikali
iangalie matukio ya uchomaji wa makanisa yanayoendelea nchi nzima.
Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa makanisa.
Alisema kanisa ni taasisi ya jamii, hivyo anaomba serikali ichangie
gharama ya ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa
hilo wapate sehemu ya kuabudia.
KANISA LA WAADVENTISTA LALAANIKanisa
la Waadventista Wasabato limetoa tamko rasmi dhidi ya tukio la
kuharibiwa kwa jengo la ibada la kanisa hilo lililoko Mbagala, jijini
Dar es Salaam na kuchomwa moto kwa makanisa mengine ya Kikristo na watu
wanaodaiwa kuwa ni waumini wa Kiislamu.
Akitoa tamko hilo mbele
ya waandishi wa habari mjini Morogoro jana, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo
Jimbo la Mashariki mwa Tanzania, Mark Malekana, alitaka serikali
kulichukulia suala hilo kwa uzito wa kipekee.
Alisema licha ya
kanisa hilo licha ya kupongeza kauli za viongozi wa madhehebu mengine ya
dini na serikali za kukemea na kulaani viendo hivyo, lakini viongozi wa
dini ya Kiislam nao wanapaswa kuwachukulia hatua za kinidhamu waumini
wao wanaohatarisha amani .
“ Lazima hawa viongozi wa dini ya
Kiislam wawachukulie hatua hao waumini ambao wameanza kuharibu amani ama
sivyo jamii itakuwa na picha isiyo sahihi,” alisema.
Askofu huyo
alisema matukio ya kushambulia na kuharibu majengo matakatifu ya ibada
ya Kikristo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na hata kusababisha
wasiwasi kwa waumini wa dini hiyo, jambo ambalo likiachwa liendelee
linaweza kuharibu amani nchini.
“Kanisa halikufurahishwa kabisa
na kitendo cha mtoto kudhalilisha kitabu kitukufu cha Kuran na
nailipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua zilizochukuliwa za kumuweka
kituoni mtoto huyo kwa uchunguzi zaidi na kwa usalama,” alisema.
Aliongeza:
“Kitendo cha kukamatwa na polisi kinaonyesha jinsi dola isivyochukulia
kirahisi mambo yayoweza kuvuruga amani miongoni mwa jamii. Kwa kweli
kitendo cha mtoto huyo ni cha aibu.”
Alisema kuwa bado kanisa
lake linalaani vitendo vya watu wazima wenye kujua sheria za nchi, tena
watu wa kiroho kuamua kuchukua hatua mkononi kwa kuvamia kituo cha
polisi na kufanya uharibifu wa makanisa ambayo hata hayakuhusika na
kitendo kilichofanywa na mtoto huyo.
“Kwa kweli vitendo hivyo
havikupaswa kabisa kutendwa na watu wanaomcha Mungu, kwani mcha Mungu ni
mtu anayetegemewa kuwa muhimili wa amani katika jamii na kutokana na
hali hiyo, ninawaomba pia viongozi wa dini ya Kiislam wawachukulie hatua
za kinidhamu hawa waumini wao wanaohatarisha amani yetu ama sivyo jamii
itakuwa na picha mbaya isiyo sahihi,” alifafanua Askofu Malekana.
Askofu huyo alisema kuwa kanisa lake limefarijika kwa kauli
zilizotolewa na viongozi mbalimbali akiwAmo Rais Kikwete; Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki; Kamanda wa Polisi Kanda na Maalum
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kwamba
zinazooneshwa kukerwa na matendo hayo na kuwataka waamini wa dhehebu
hilo na Watanzania kwa ujumla kuwa wavumilivu wakati serikali
ikishughulikia suala hilo.
Alisema Kanisa la Waadiventista
Wasabato haliwezi kutafuta haki kwa kuvunja sheria, bali linapoona kuwa
halitendewi inavyostahili, huitafuta haki kwa mujibu wa sheria.
Katika
vurugu zilizotokea Oktoba 12, Mbagala jijini Dar es Salaam, jumla ya
makanisa saba yalichomwa moto na mengine kuharibiwa na kikundi cha watu
wanaotumia kivuli cha dini ya Kiislam kufanya vurugu hizo.
MBATIA: TUJADILI MUSTAKABALIMwenyekiti
wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amemuomba Rais Jakaya Kikwete
kuwakutanisha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam pamoja na
wanasiasa ili kujadili namna ya kumaliza chuki inayozuka kati ya dini
hizo mbili.
Mbatia alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mstakabali wa vurugu
zilizojitokeza wiki iliyopita huko Mbagala, baada ya kwa waumini wa
Kiislam kuchoma makanisa kufuatia kijana mmoja wa anayedaiwa kuwa
Mkristo kukojolea Kuran.
Mbatia alisema tukio hilo siyo jambo la
kuchukulia kibusara eti kwamba lilisababishwa na watoto, bali kutafuta
ufumbuzi wa chanzo cha matatizo hayo.
“Vitendo hivi havijaibuka
jana wala juzi, tumeshuhudia mara kadhaa makanisa yakichomwa hata
Zanzibar tumeshuhudia, hivyo watoto nao wanajifunza kutoka kwa wakubwa
kwamba chuki ipo kati ya pande hizo, tusisubiri itokee kama nchi za
wenzetu kwa sababu nao walianza hivi hivi,” alisema.
Mbatia
ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, aliongeza: “Tunaiomba serikali
isifumbie macho jambo hili, bali ichukue jukumu la kuwakutanisha
viongozi wa dini hizo pamoja na wanasiasa kuzungunguza kwa pamoja na
kuangalia namna ya kumaliza chuki iliyopo hivi sasa.”
Alisema ni
jambo la kushangaza kuona viongozi wa dini na wanasiasa wamenyamaza na
pasipo kusema jambo lolote kuhusiana na vurugu zinazojitokeza.
“Ni
jambo la kushangaza kuona kwamba hali inazidi kuwa tete, lakini wenye
kuchukua maamuzi na kukemea wamekaa kimya, ni shetani gani ameingilia
nchi hii au wana lao jambo?” alihoji.
Aidha, alisema baadhi ya
wanasiasa nao wamekuwa ni kichocheo cha kujenga matabaka ya udini na
kwamba kitendo hicho kinatakiwa kukemewa mara moja.
126 KORTINI LEOWatu
126 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Dar es Salaam
kufuatia vurugu zilizotokea katika eneo la Mbagala Kizuiani wiki
iliyopita ambazo zilisababisha kuchoma moto makanisa na kuharibu mali.
Vurugu hizo zilisababishwa na kitendo mtoto wa miaka 14 kukojolea kurani.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alisema jana kuwa askari polisi
waliendelea na msako ili kubaini wahalifu katika tukio hilo, hata
hivyo, alisema kuwa walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine sita
juzi.
“Unajua jana asubuhi nilikuwa kwenye kikao kujadili suala
hilo na kuamua kuwa muda wowote kuanzia leo (jana) watuhumiwa wote
watakufikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria zitakamilika,”
alisema Misime.
Watu hao wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani
imedaiwa kuwa ni waumini wa dini ya Kiislam, waliovamia makanisa manne
na kuyakuchoma moto, kwa madai kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 14
alikojolea kitabu cha Kurani tukufu.
Kufuatia vurugu hizo, mali
mbalimbali ziliharibiwa ikiwa ni pamoja vifaa vya kuendeshea ibada, vioo
vya magari vilivunjwa, hasara kamili ya uharibifu huo haijafahamika.
Rais
Kikwete katika hotuba yake juzi ya kuzima mbio za Mwenge wa uhuru na
Kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, aliwataka viongozi wa dini hizo na waumini wao kuwa watulivu na
wavumilivu wakati Jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi. Pia alisema
wahusika wa vurugu hizo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.